Image caption Rais mteule wa Marekani Donald Trump amesema kuwa ataimarisha uhusiano na taifa la Urusi

Donald Trump ameshiriki mazungumzo kwa njia ya simu na rais wa Urusi Vladmir Putin.

Kulingana na taarifa kutoka kwa ofisi ya bwana Trump, ameeleza matumaini, ya kuwa na uhusiano dhabiti na wa kudumu na Urusi.

Taarifa kutoka Kremlin imesema kwamba wamekubaliana kushirikiana ili kulainisha uhusiano na Marekani.

Wawili hao aidha wamejadili umuhimu wa kushirikiana katika vita dhidi ya ugaidi.

Uhusiano kati ya Urusi na Marekani ulisambaratika baada ya Urusi kunyakua Crimea mwaka wa 2014, jambo lililopelekea Marekani kuweka vikwazo dhidi ya Urusi.

Vita vinavyoendelea nchini Syria pia vimezorotesha ushirikiano bain ya mataifa hayo.

Image caption Rais mteule wa Marekani Dolad Trump na rais wa Marekani Barrack Obama

Wakati huohuo Rais Barack Obama amewahakikishia washirika wa Marekani kwamba Donald Trump ataendeleza heshima na ushirikiano wa kimataifa baina ya nchi yake nao wakati yeye atakapokabidhi urais mwezi Januari.

Obama ameyasema hayo wakati alipokuwa na mkutano mkubwa na waandishi habari .

Rais Obama amesema kwamba Donald Trump ameonesha nia ya kutaka kudumisha uhusiano baina ya Marekani na shirika la kujihami la NATO.

Obama amesema kwamba Marekani lazima iendelee kuwa nguzo ya nguvu na nguzo ya matumaini kwa watu duniani kote.

Na kuongeza kusema kwamba uhusiano baina ya nchi na nchi unakwenda mbali zaidi ya nafasi ya urais na wanadiplomasia,majeshi na kwamba wakuu wenye hekima na busara wataendelea kuonesha ushirikiano na wenzao wanaoshughulikia masuala ya kigeni.

Obama alikuwa akizungumza kuelekea mwishoni mwa safari zake za mataifa ya kigeni akiwa mwishoni mwa madaraka yake ya urais.